Header

Katika kijitabu hiki tutatazama ni nini Biblia inafunza kumhusu Bwana Yesu Kristo.

 

Bwana Yesu Kristo na kazi yake ndiyo msingi wa ukristo.  Bila Bwana Yesu Kristo hakuna ukristo, ni kama kuutoa moyo kutoka kwa mwili wa mwanadamu.  Kwa hivyo ni muhimu sana kusoma mafunzo haya kwa uangalifu sana.  Usijiambie kwamba, “Ninajua yote ambayo nafaa kujua kumhusu Bwana Yesu Kristo,” kwa sababu ni mapenzi ya Mungu tubadilishwe katika mfano wa Kristo.  Hakikisha kwamba unasoma mafundisho haya na moyo ambao umenyenyekea na ambao uko tayari kufunzwa.

 

Katika mafunzo haya tutajifunza kutoka vifungu vitatu katika Agano Jipya: Yohana 1:1-18, Waebrania 1:1-3, Wafilipi 2:3-11.  Kila funzo limeandikwa kufunza jambo fulani kutoka kwa Biblia.  Kabla hujasoma funzo, tafadhali hakikisha umesoma kifungu kutoka kwa Biblia ambacho funzo hilo linatoka.

 

Masomo katika kitabu cha Yohana 1:1-18.

 

Funzo la Kwanza: Tafadhali Soma Yohana 1:1-3.

 

Katika mistari hii mitatu tunajifunza mambo haya kumhusu Bwana Yesu Kristo.

 

1.  Bwana Yesu Kristo ni Mungu.

 

Huu ndiyo ujumbe muhimu wa injili hii ya Yohana.  Katika kitabu cha Yohana mara kwa mara anaendelea kutuonyesha kwamba Bwana Yesu Kristo ni Mungu.  Katika mistari hii mitatu ya kwanza Yohana anatuambia kwamba Bwana Yesu Kristo ni Mungu kwa njia tatu.

 

(i) Anasema kwamba, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno.”  Yohana anazungumza kuhusu Bwana Yesu Kristo akimwita “Neno,” na anaanza katika kitabu chake akisema kwamba Bwana Yesu Kristo alikuwako mwanzoni.  Hii inamaanisha kwamba yeye ni Mungu kwa sababu tunajua kwamba ni Mungu tu peke yake ambaye amekuwako tangu mwanzoni.  Hadi Mungu alipoumba ulimwengu na mbingu hakukuwa na chochote wala mtu yeyote isipokuwa Mungu.  Mungu amekuwako tangu mwanzoni na ataendelea kuwako; Mungu ni wa milele.  Kwa hivyo wakati Yohana anatuambia kwamba Bwana Yesu Kristo alikuwako tangu mwanzoni, anatuambia kwamba Bwana Yesu Kristo ni Mungu.

 

(ii) Yohana anatuambia wazi kwamba Bwana Yesu ni Mungu.  Anasema kwamba, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwa kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.”  Mara mingi tunakutana na watu nchini mwetu ambao wanakataa kwamba Bwana Yesu Kristo ni Mungu.  Hawa ni watu wa dhehebu la mashahidi wa Yehovah na huwa wanawatembelea watu katika manyumba zao wakiwapatia makaratasi kuhusu dhehebu lao.  Dhehebu hili limetafsiri Biblia kwa njia yao  kuambatana na mafunzo yao.  Mstari huu wameutafsiri kwamba Yesu ni mungu fulani bali Yeye si Mwenyezi-Mungu.  Je, kwa nini watu hawa wanatafsiri mstari huu hivi?  Ni kwa sababu kulingana na mafunzo yao Bwana Yesu Kristo siyo Mungu.  Kwa hivyo kile wamefanya ni kuanzisha mafunzo ambayo hayapatikani katika Biblia.  Wakati wanakutana na mstari katika Biblia ambao uko kinyume na mafunzo yao, wanaubadilisha mstari huo ili uweze kusomeka kulingana na mafunzo yao.  Lakini Biblia ni wazi kwamba Bwana Yesu Kristo ni Mungu.

 

(iii) Yohana anatuambia kwamba Bwana Yesu Kristo ndiye aliyeumba kila kitu.  “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika.”  Yohana anatuambia kwamba kila kiumbe kiliumbwa na Bwana Yesu Kristo.  Kwa kusisitiza jambo hili anasema kwamba hakuna chochote kilichofanyika bila Yeye.  Aliandika hivi ili watu wasiseme kwamba, “Kuna vitu vichache ambavyo hakufanya.”  Yohana anasema wazi kwamba kila kitu ambacho tunaona karibu na mbali nasi, kiliumbwa na Bwana Yesu Kristo.  Huu ni ukweli mtupu kwamba Bwana Yesu Kristo ni Mungu.  Biblia ni wazi kwamba ni Mungu ambaye aliumba kila kitu (Mwanzo 1:1).  Ni Mungu tu peke yake ambaye angeumba ulimwengu.  Hakuna mtu au malaika angeumba ulimwengu, jua, mwezi na nyota na mambo mengine yote.

 

2.  Bwana Yesu Kristo ndiye ujumbe wa Mungu kwetu.

 

Yohana anamwita Bwana Yesu Kristo, “Neno.”  Sisi huzungumza kwa maneno na pia Mungu huzungumza kwa maneno; Biblia inaitwa Neno la Mungu kwa sababu ni Mungu anazungumza.  Yohana anamwita Bwana Yesu Kristo “Neno” kutueleza kwamba Mungu hajanyamanza.  Hajamwacha mwanadamu bila kumfahamu yeye ni nani, kwani amezungumza nasi kupitia kwa Mwanawe (Waebrania 1:1-2).

 

Hii ni kazi ya neema ya Mungu.  Sisi ni wanadamu tu ambao hatuelewi kila kitu.  Ni ukweli kwamba wanadamu ni werevu sana na wako na uwezo wa kufanya mambo makubwa sana.  Lakini hii haimaanishi kwamba tuko na akili yote ya kujua kila kitu.  Ukweli ni kwamba hata kama tuko na uwezo fulani wa kufanya mambo fulani, sisi ni wanadamu tu na kuna mambo mengine ambayo hatuwezi kufanya au kujua.  Pia sisi ni wanadamu ambao wameanguka katika dhambi na dhambi imedhuru mawazo yetu sana.  Hivi ndivyo Biblia inavyofafanua hali ya mwanadamu: “Akili zao zimetiwa giza, nao wamefarikishwa na uzima wa Mungu, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao” (Waefeso 4:18).

 

Hii inamaanisha kwamba hadi Mungu atuokoe hatuwezi kuokolewa.  Kila mwanadamu ako na mawazo yake kumhusu Mungu na jinsi alivyo, lakini mawazo yake yameharibiwa na dhambi na mawazo yake ni uongo.  Mtu anaweza kusema jambo kama hili, “Mimi nimejitolea kwa Mungu katika maombi na kuhudhuria kanisa kila juma.  Kwa sababu ya haya Mungu atanipatia kazi mzuri na atanilinda kutokana na magonjwa.”  Lakini haya ni mawazo ya uongo kumhusu Mungu na jinsi alivyo; hili silo jambo ambalo Mungu amesema mahali popote katika neno lake.  Shida kubwa ambayo tuko nayo leo katika ulimwengu ni kwamba watu wengi wako na mawazo yao kumhusu Mungu na jinsi alivyo na ahadi zake na jinsi anavyofanya kazi yake. Halafu watu hawa wanahubiri jinsi wamewaza bali siyo kulingana na neno la Mungu.  Watu hawa hawasomi na kujifunza Biblia kwa uangalifu lakini wanafunza na kuhubiri mawazo yao wenyewe.  Haya ni makosa makubwa kwa sababu wanakataa neno la Mungu na kuhubiri uongo katika jina la Mungu. Wanasahau kwamba Mungu amejitambulisha kwetu kupitia kwa Mwanawe.  Yesu alisema, “Aliyeniona mimi amemwona Baba” (Yohana 14:9).  Jukumu letu kubwa ni kusoma na kujifunza kuhusu maisha na mafundisho ya Bwana Yesu Kristo kwa sababu Yeye ndiye Neno.

 

3.  Bwana Yesu Kristo siye Mungu Baba.

 

Yohana katika kifungu hiki anaandika, “Naye Neno alikuwako kwa Mungu.”  Mstari huu unafunza wazi kwamba kuna Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo.  Wote wawili kila mmoja ni Mungu kamili.  Siyo ukweli kwamba kuna Mmoja ambaye anajitambulisha kuwa Baba au Mwana au Roho.  Ni mawazo ya watu wengi leo nchini mwetu kwamba Mungu katika Agano la Kale alijitambulisha kama Baba na katika vitabu vinne vya Injili (Mathayo, Marko, Luka na Yohana) amejitambulisha akiwa Mwana na katika kitabu cha Matendo ya Mitume hadi leo anajitambulisha kama Roho Mtakatifu.  Jambo hili si la ukweli.  Biblia inatufunza kwamba kuna Mungu Mmoja ambaye anaishi milele akiwa katika Utatu; Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.  Kila Mmoja wao ni Mungu kamili.  Baba siyo Mwana na Mwana siyo Roho Mtakatifu.

 

4.  Bwana Yesu Kristo ako katika ushirika wa karibu sana na Mungu Baba.

 

Mstari huu unasema, “Neno alikuwako kwa Mungu.” Hii ni dhihirisho kwamba kuna ushirika wa karibu sana kati ya Mungu Baba na Mwana.  Mstari huu unaweza kutafsiriwa, “Neno alikuwa uso kwa uso na Mungu Baba.”  Biblia inafunza wazi kwamba Utatu wa Mungu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wote wako na umoja, amani na ushirika wa pamoja.  Hata kama kila Mmoja ni Mungu kamili kivyake, wote wanafanya kazi pamoja.

 

Ukweli huu unapatikana wazi katika mpango wa Mungu wa wokovu.  Biblia inatufunza kwamba mpango wa wokovu ulipangwa kwa uangalifu sana na Mungu wa Utatu.  Biblia inasema “Kama vile Mungu Baba alivyotangulia kuwajua katika kutakaswa na Roho, hata mkapata kutii na kununyiziwa damu ya Yesu Kristo” (1 Petro 1:2).  Katika mstari huu tunaona kwamba wokovu wetu ulipangwa kwa uangalifu sana na Mungu wa Utatu.  Kila Mmoja wa Utatu alikubali kufanya kazi fulani ndipo tuokolewe.  Mungu Baba alituchagua tuokoke, Mungu Mwana alimwaga damu yake ili atuoshe kutokana na dhambi zetu na Mungu Roho Mtakatifu anafanya kazi ndani mwetu ya kututenga kutoka kwa ulimwengu.  Baada ya kutuokoa Roho Mtakatifu anaendelea kutoa dhambi ambazo ziko ndani mwetu.  Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu wanafanya kazi pamoja kutuokoa.

Funzo La Pili:  Tafadhali Soma Yohana 1:4-5.

 

Katika mistari hii tunajifunza haya kumhusu Bwana Yesu Kristo.

 

1.  Bwana Yesu ako na uzima ndani mwake.

 

Yohana anasema katika mstari wa 4, “Ndani mwake ndimo ulimokuwa uzima.”  Yohana anapozungumza kuhusu uzima, hazungumzi kuhusu uzima wa mwili ambao watu wako nao hapa ulimwenguni.  Yohana anazungumza kuhusu maisha ya kiroho, yaani wokovu.  Jambo hili ni wazi katika kifungu kimoja ambacho kinapatikana katika kitabu hiki.

 

“Amini, amini, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini Yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.  Amini, amini, nawaambia saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai.  Maana kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake.  Naye akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu” (Yohana 5:24-27).

 

Biblia inafunza kwamba wale wote ambao hawajaokoka hawana maisha ya kiroho (Waefeso 2:1), na wale ambao wameokolewa kupitia kwa Bwana Yesu Kristo wako na uzima wa kiroho.  Hii ndiyo sababu Biblia inasema kwamba, “Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima” (1 Yohana 5:12).

 

Kile Yohana anasema hapa ni kwamba kuna mmoja tu ambaye anaweza kutupatia wokovu, naye ni Bwana Yesu Kristo.  Ulimwenguni leo kuna wale ambao hudai kwamba wanaweza kuwaokoa watu; lakini Biblia ni wazi kwamba Bwana Yesu Kristo ndiye anaweza peke yake kutupatia wokovu.

 

(i) Kuna watu katika ulimwengu leo ambao husema kwamba wokovu unapatikana kwa kila dini. Kwa hivyo wanasema kwamba kila mmoja ambaye ako kwa dini anaabudu Mungu wa ukweli, kwa sababu wamejitolea kwa matendo ya kidini na kuamini yale ambayo wanaamini.  Lakini Biblia inasema kwamba ni wale tu ambao wanakuja kwa Bwana Yesu Kristo kwa imani wakitubu dhambi zao, ndiyo wataokolewa.

 

(ii) Kuna watu leo ambao wanasema kwamba wanaweza kuokolewa kutokana na matendo yao mazuri.  Wanaamini kwamba wakijitahidi sana kutii Sheria Kumi za Mungu na kuenda kanisani kila Jumapili, basi wataingia mbinguni kwa sababu ya kujitahidi kwao.  Biblia haifunzi jambo hili kamwe.  Tunaokolewa na Bwana Yesu Kristo peke yake bali si kwa matendo yetu mazuri au kuzingatia sheria

 

(iii) Kuna watu wengine pia ambao wanasema kwamba wanaweza kuokolewa na mchungaji au kasisi.  Wanaamini kwamba kasisi ako na mamlaka ya kusamehe dhambi, na kwa hivyo wanapeleka dhambi zao kwake.  Wengine wanafikiria kwamba wakirudia maombi fulani ambayo mchungaji anawaambia au mchungaji akiwawekelea mikono na kuwaombea, wataokolewa.  Kufanya jambo hili ni kuamini kwamba mwanadamu anaweza kukuokoa.  Mambo haya yote hayatufaidi,  Yesu Kristo peke yake ndiye ako na mamlaka ya kutuokoa.

 

Hatuokolewi kwa sababu ya kujitahidi sana au kwa sababu ya uamuzi wetu au kwa sababu ya mtu mwingine yeyote.  Wokovu haupatikani kwa njia yoyote ile, bali ni kwa Bwana Yesu Kristo pekee: “Ndani mwake kulikuwako na uhai.”  Ni Bwana Yesu pekee ambaye anatuokoa sisi watenda dhambi na anatuokoa kulingana na mpango wake.

 

2.  Uzima wa Bwana Yesu Kristo ndiyo nuru ya wanadamu.

 

Yohana anasema katika mistari ya 4-5 kwamba, “Ndani mwake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu.  Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza.”  Kuna mambo mawili ambayo Yohana anatufundisha hapa.

 

(i) Bwana Yesu Kristo ndiye nuru ya wanadamu.  Baadaye katika injili hii, Yohana anaeleza jambo hili linamaanisha nini.  Yohana anasema “Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru ilikuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu.  Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa.  Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu” (Yohana 3:19-21).  Kile Yohana anasema hapa ni kwamba Bwana Yesu Kristo ndiye  nuru ya ulimwengu na anafunua wazi dhambi za ulimwengu.  Kama vile mwangaza huonyesha sehemu za nyumba zilizo na uchafu, vivyo hivyo Bwana Yesu Kristo huonyesha wazi matendo ya dhambi za walimwengu.  Hii ndiyo sababu wale hawajaokoka hawawezi kuja kwake hadi Roho Mtakatifu awalete.  Wanakataa kuja kwa sababu hawataki matendo yao mabaya yaonekane wazi.

 

(ii) Yohana anasema giza halishindi nuru nguvu.  Ijapokuwa dunia na wenye dhambi waliomo wanamchukia Kristo na wanakataa kuja kwake, hawawezi kuondoa nuru yake. Nuru ya Kristo huonyesha wazi dhambi zao na inazungumzia hata dhamira zao.  Wenye dhambi hawawezi kuishinda nguvu nuru ya Kristo ama kumnyamazisha Kristo.  Kristo ataendelea kuonyesha dhambi zao wazi na mwishowe Kristo atawahukumu kwa sababu ya matendo yao mabaya.

 

 

 

Funzo La Tatu: Tafadhali Soma Yohana 1:10-13.

 

Katika mistari hii Yohana anaendelea kutupatia mafunzo kumhusu Bwana Yesu Kristo.

 

1.  Bwana Yesu Kristo alikuwako katika ulimwengu.

 

Yohana anasema kwamba, “Alikuwako ulimwenguni.”  Huu siyo wakati pekee ambapo Mungu alikuwako ulimwenguni.  Katika Mwanzo 3:8 tunasoma kuhusu Mungu akitembea katika bustani la Edeni wakati wa mchana.  Katika Mwanzo 18:17 tunasoma kwamba Mungu alimtembelea Ibrahimu na Sara.  Katika kitabu cha Kutoka 12:12 tunasoma kwamba Mungu alipita katika nchi ya Misri.  Ukweli ni kwamba mara kwa mara Mungu ametembea hapa ulimwenguni.  Hii inaonyesha mambo mawili muhimu.

 

(i) Kwanza, inatuonyesha kwamba Mungu anashughulika sana na yale yote ambayo yanatendeka hapa ulimwenguni.  Wakati Adamu na Hawa walianguka katika dhambi Mungu angeweza kujiondoa kabisa katika shughuli za ulimwengu huu.  Lakini Mungu hakufanya hivyo.  Mungu aliendelea kutembelea ulimwengu kuonyesha kwamba alikuwa bado na shughuli na viumbe vyake.

 

(ii) Pili, inatuonyesha kwamba Mungu ako na mipango mikubwa kwa ajili ya ulimwengu.  Biblia inatuambia kwamba siku moja Mungu amepanga kuondoa laana ya dhambi kutoka kwa viumbe vyake na kuvifanya vipya tena.  Yesu Kristo alikuwako hapa ulimwenguni na hii ni dhihirisho kwamba siku moja atafanya kila kitu kuwa kipya.

 

2.  Ulimwengu haukumtambua.

 

Huu ni mstari muhimu sana wa kuzingatiwa.  Mungu mwenyewe alitembelea ulimwengu na watu wa Mungu hawakumtambua.  Ni jambo la huzuni kwamba alikuja kwa watu wake lakini watu wake hawakumtambua.  Alikuja kwa Waisraeli, watu ambao walipewa Agano la Kale, na  kwa sababu walipewa Agano hili, walitakikana wamtambue mara moja.

 

(i) Katika Agano la Kale Mungu anajitambulisha kwetu jinsi alivyo na jinsi anavyofanya kazi. Ukweli ni kwamba wakati tunasoma Agano la Kale tunaona kwamba ni Mungu ambaye anajitambulisha kwetu.

 

(ii) Katika Agano la Kale Mungu aliwaambia Waisraeli kwamba siku moja angekuja katika ulimwengu.  Agano la Kale liko na unabii kuhusu kuja kwake Yesu Kristo katika ulimwengu.  Ni wazi kwamba wakati Herode alitaka kujua ni wapi Yesu amezaliwa, viongozi wa kidini wa Waisraeli waliweza kumwambia kwa haraka (Mathayo 2:4-5).

 

(iii) Mungu aliwaambia Waisraeli kusudi lake la kuja katika ulimwengu; siyo kuanzisha ufalme wa kidunia bali ufalme wa kiroho, yaani ufalme ambao utasambaa kwa kila pembe ya ulimwengu (Danieli 2:44).

 

Hata baada ya mambo haya yote, Waisraeli hawakumtambua Mungu wakati alipokuja katika ulimwengu.  Kwa nini?  Ni kwa sababu dhambi inatufanya tuwaze mambo ya uongo kumhusu Mungu na ukristo wa ukweli.  Waisraeli walikuwa wamewaza kwamba wakati mwokozi atakapokuja, atawafukuza Warumi kutoka nchi yao na ajijengee ufalme wake katika mji wa Yerusalemu.  Waisraeli walitaka kiongozi wa siasa.  Mawazo ya mtenda dhambi yanawaza tu mambo ya ulimwengu siyo ya kiroho.  Mawazo ya mtu huyu huwaza tu juu ya anasa na mali ya ulimwengu huu tu, hayawazi kuhusu wokovu na ufalme wa Mungu.  Mambo haya hayapatikani katika fikira zao.

 

Mambo haya ni ya kawaida nchini mwetu leo.  Watu leo hawasomi Biblia ili wajue jinsi Mungu alivyo na ni kazi gani anafanya katika ulimwengu leo.  Wanasoma Biblia wakiwa na mawazo yao ya uongo.  Wanafikiria kwamba Mungu ako kwa sababu ya faida yao na kwamba wakiwa na tabia mzuri na wawe wamejitolea katika kazi ya Mungu, basi atawabariki na mali nyingi.  Makanisa mengi leo hawajali na mambo ya ufalme wa Mungu, bali wanajali tu utajiri na mali ya ulimwengu.  Jinsi Waisraeli katika nyakati za Yesu hawakumtambua, ndivyo ilivyo leo watu hawamjui Mungu jinsi alivyo, hata wale ambao wanadai kuwa wameokoka.

 

3.  Ulimwengu haukumpokea.

 

Kwanza Yohana anasema kwamba ulimwengu haukumtambua halafu anaendelea kusema kwamba ulimwengu haukumpokea.  Mara mingi tunawapokea watu ambao hatuwaelewi.  Mtu anapobisha mlango, mwenye nyumba anaweza kukosa kuelewa mtu huyo, lakini bado anaweza kumkaribisha ndani ya nyumba na akamshughulikia.  Lakini ulimwengu haukuweza kumkaribisha Bwana Yesu miongoni mwao.  Haukujua Yeye ni nani na haukumkaribisha au kumpokea.

 

Jambo hili linatuonyesha madhara ya dhambi ya Adamu kwa mwanadamu.  Wakati Adamu na Hawa walipoanguka dhambini, walijificha nyuma ya mti kwa sababu hawakutamani tena ushirika na Mungu (Mwanzo 3:8).  Walitaka kuwa huru kutoka kwa Mungu na hawakutaka Mungu ajishughulishe na mambo yao.  Ni kama ule mfano wa mtoto mpotevu (Luka 15:11-31).  Mtoto alikuwa anakaa ndani ya nyumba ya babake lakini hakutaka kuendelea kuishi katika nyumba hiyo.  Alijihisi kwamba katika nyumba ya babake hangeweza kufanya kile anataka kufanya.  Hakutaka babake ajishughulishe na mambo ya maisha yake; alitaka awe huru afanye yale yeye mwenyewe alitaka kufanya.  Hii ndiyo imekuwa hali ya mwanadamu tangu kuanguka kwa Adamu na Hawa.  Huwa tunapata kwamba Sheria ya Mungu ni ngumu sana kwetu na inatuzuia kufanya yale tunataka kufanya.  Tunataka kuishi maisha ya dhambi hapa ulimwenguni na hatutaki sheria zake au njia zake zituzuie.

 

Fikiria juu ya kikundi cha wanaume ambao wako katika chumba kimoja na wako na pombe na haja yao ni kunywa pombe hiyo.  Mgeni anakuja na kubisha mlango kwa sababu anataka  kuungana nao katika kunywa.  Hata akiwa ni mtu ambaye hawamjui, watampokea.  Lakini ikiwa mgeni yule ni mchungaji wa kanisa la Mungu hawatafurahi kumwona.  Ikiwa mchungaji ataingia, mahali pale kutakuwa na kimya cha ubaya, na wakati atakapoondoka watacheka sana na wataendelea na pombe yao.  Au pia wanaweza kukosa kumkaribisha yule mchungaji ndani ya nyumba na waseme kwamba, “Tuko na shughuli kwa wakati huu, labda unaweza kurudi wakati mwingine.”  Watu wa ulimwengu hawampokei Kristo Yesu kwa sababu wako ndani ya dhambi.  “Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu.  Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa” (Yohana 3:19-20).

 

4.  Kwa wale ambao waliompokea, aliwapa uwezo kuwa wana wa Mungu.

 

Yohana anasema kwamba ulimwengu haukumpokea.  Lakini kuna watu kadhaa ambao walimpokea.  Katika mistari ya 12-13 Yohana anatupatia mafunzo muhimu sana kuhusu jambo hili.

 

(i) Je, inamaanisha nini kumpokea Kristo?  Yohana anasema kwamba, “Bali wote waliompokea ...ndio wale waliaminio jina lake.”  Kumpokea Kristo inamaanisha kuweka imani yako ndani mwake.  Kuna mamilioni leo ulimwenguni ambao wanajiamini na matendo yao kuwa yatawapeleka mbinguni.  Wanajiwazia kwamba watakaposimama kwa milango ya mbinguni, wataeleza kwamba hapa ulimwenguni waliishi maisha mazuri na yenye tabia mzuri na pia walienda kanisani.  Wanajiwazia kwamba matendo yao na yale ya kidini yatawapeleka mbinguni.  Hawaoni kwamba kwa kuamini matendo yao wanamkana Kristo Yesu.  Kristo anawaalika waje kwake awapatie msamaha kamili na wa bure wa dhambi zao kupitia kwa damu yake. Lakini watu wanaona vyema kuendelea kuamini matendo yao.  Lakini kuna wengine ambao humpokea Kristo Yesu na kumwamini ili awaokoe.  Tumaini lao la kuingia mbinguni haliko katika matendo yao mazuri au yale ya kidini bali ni kwa Bwana Yesu Kristo.  Wanaamini kwamba kupitia kwa kifo na kufufuka, Bwana Yesu Kristo amefanya yale yote ambayo yanahitajika kuwapeleka mbinguni.

 

(ii) Je, nini hutendeka kwa wale wote ambao humpokea Bwana Yesu Kristo?  Yohana anasema kwa wale wote ambao walimpokea, “Aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.”  Kwa wale wote ambao wanakuja kwa Bwana Yesu Kristo kwa imani na kumwamini kwa wokovu wao wanafanyika watoto wa Mungu.  Hili ni kumbusho kubwa kwetu kuhusu jinsi wokovu ni kitu cha maana sana.  Wakati tunapokuja kwa Yesu atuokoe, anatusamehe dhambi zetu na kutuosha, na pia anatufanya kuwa watoto wa Mungu.

 

(iii) Je, tunafanyika aje watoto wa Mungu?  Katika mstari wa 13, Yohana anasema kwamba wale wote ambao wameokolewa, “Si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.”

 

Yohana anasema kwamba mtu hazaliwi katika jamii ya Mungu kwa mapenzi ya mtu.  Hii inamaanisha kwamba ikiwa wazazi wa mtoto wameokoka, kwa hivyo mtoto huyu hafanyiki mtoto wa Mungu kwa sababu amezaliwa na wazazi ambao wameokoka.  Mtoto huyu ni mwenye dhambi kama tu yule ambaye amezaliwa na wazazi ambao hawajaokoka.   Kwa sababu wazazi wa mtoto huyo wameokoka, hii haimfanyi mtoto huyo kuwa mtoto wa Mungu.  Njia moja tu mtoto huyu anaweza kuwa mtoto wa jamii ya Mungu ni kuokoka.

Mtu hazaliwi katika jamii ya Mungu kwa mapenzi yake au ya mtu mwingine yeyote.  Ni Mungu mwenyewe anaamua wokovu wa mtu, Mungu ndiye mwenye uwezo katika wokovu.

 

Mtu hazaliwi kwa jamii ya Mungu kwa uwezo wa mwanamume.  Katika mila zingine, bibi analazimika kukubali dini ya mume wake.  Yaani ikiwa mwanamke alizaliwa na wazazi  ambao ni wa kiangilikana na aolewe na mume mkatoliki basi anastahili aingie dini ya katoliki.  Haya yanafanyika tu kwa dini za huku duniani, lakini haifanyiki katika ufalme wa Mungu.  Mtu ambaye ameokoka hawezi akasema, “Nitaoa mwanamke ambaye hajaokoka na baadaye ataokoka kwa sababu kulingana na mila zetu ni lazima atimize masharti ya imani yangu.”  Mwanamke hawezi akaokoka kwa sababu ameoa mwanaume ambaye ameokoka.  Ni hatia kwa mtu ambaye ameokoka kumwoa mtu ambaye hajaokoka.

 

Mtu huzaliwa katika jamii ya Mungu wakati amezaliwa upya.  Yohana anasema “Waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.”  Mtu   anazaliwa upya wakati Mungu kupitia kwa Roho Mtakatifu anamfanya azaliwe upya.

 

 

 

Funzo La Nne: Tafadhali Soma Yohana 1:14.

 

Hii ni mojawapo ya mistari muhimu sana katika Biblia yote.  Inasema, “Naye neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”  Katika funzo hili tutaona mambo matatu ambayo yanapatikana katika mstari huu.

 

1.  Bwana Yesu alikuwa Mungu kamili na pia ni mwanadamu kamili.

 

Yohana anasema, “Naye neno alifanyika mwili.”  Kama vile tumeona katika msitari wa 1, Bwana Yesu Kristo ni Mungu kamili.  Katika mstari huu, Yohana anatueleza kwamba yule alikuwa Mungu kamili pia alikuwa mwanadamu.  Bwana Yesu ni Mungu kamili na pia ni mwanadamu kamili akiwa mtu mmoja wakati moja.  Biblia inatuambia kwamba wakati watu walimwangalia Yesu Kristo akiwa humu duniani, walikuwa wakimwangalia Mungu mwenyewe na pia mwanadamu kamili.  Bwana Yesu Kristo hakuwa tu kama mwanadamu au nusu mwanadamu bali alikuwa mwanadamu kama sisi.  Yesu alikuwa na hali yote ya binadamu kila wakati na alikuwa na hali yote ya Mungu kila wakati.  Bwana Yesu Kristo hakuacha kuwa Mungu wakati alikuwa huku duniani.

 

(i) Yesu Kristo alikuwa mwanadamu kamili ili atuokoe kutoka kwa dhambi zetu.  Biblia inasema, “Basi kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani Ibilisi” (Waebrania 2:14).  Mwandishi wa Waebrania anasema hapa kwamba kwa sababu sisi ni wanadamu kamili, Bwana Yesu Kristo alikuwa mwanadamu kamili ili kupitia kifo chake msalabani aweze kumwangamiza Ibilisi na atuweke huru kutoka kwa utumwa wa dhambi.  Hii ndiyo sababu ilikuwa ni lazima Yesu awe mwanadamu kamili, kwa sababu alikuja kuokoa wanadamu kutoka kwa dhambi zao, na njia ya pekee ya kukubalika kuwa dhabihu kamilifu ni awe mwanadamu kamili.

 

(ii) Yesu Kristo alikuwa awe mwanadamu kamili ili awe kuhani mkuu mkamilifu.  Mwandishi wa Waebrania anasema “Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu, bali yeye aliyejaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote , bila kufanya dhambi.  Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji” (Waebrania 4:15-16).  Bwana Yesu Kristo alienda mbinguni kuanza kazi ya kuhani mkuu.  Wakati huu Bwana Yesu Kristo anatuwakilisha kwa Mungu, anatuombea na kufanya maombi yetu na ibada zetu kukubalika na Mungu.  Njia moja ya kutimiza haya kikamilifu ni kuwa mwanadamu kamili.  Ni lazima aelewe udhaifu na shida za wale anaowawakilisha.  Hii ndiyo sababu Biblia inasema tuko na kuhani mkuu ambaye alijaribiwa jinsi tunavyojaribiwa.

 

(iii) Bwana Yesu Kristo alikuwa awe mwanadamu kamili ili awe kielelezo cha ufufuo wetu.  Paulo anasema “Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu limbuko lao waliolala.  Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu.  Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa.  Lakini kila mmoja mahali pake; limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja” (1 Wakorintho 15:20-23).  Biblia inatufunza kwamba wakati Yesu atarudi, tutakuwa na miili ya ufufuo.  Sababu ya Yesu kuwa mwanadamu kamili ni kwamba awe kielelezo cha ufufuo wetu: kile kilimfanyikia yeye kitatufanyikia nasi, Yeye alikuwa limbuko na kielelezo cha ufufuo wetu.

 

2.  Bwana Yesu Kristo alikaa miongoni mwetu.

 

Yohana anasema katika msitari huu “Naye neno ilifanyika mwili, akakaa kwetu.”  Bwana Yesu alikuja na akaishi miongoni mwetu na angali anaendelea na kukaa na watu wake kupitia kwa Roho Mtakatifu.  Kwa namna nyingi hatuko tofauti na watu wa Mungu wakati Bwana Yesu alikuwa nao humu duniani.  Bwana Yesu alikuja kuwaita watu wake kutoka kwa giza ya dhambi na kuwapeleka kwa ufalme wa nuru wa Mungu ndiyo awatakase na kuwarekebisha ili wawe tayari kwa makao yao ya milele naye.  Hii ndiyo kazi Bwana Yesu anaendelea kufanya kupitia kwa Roho Mtakatifu hapa ulimwenguni leo.  Anawaita wenye dhambi kutoka kwa giza na anawaingiza kwa ufalme wa nuru, na kupitia kwa Roho Mtakatifu anawatakasa na kuwarekebisha ili atakaporudi wawe tayari.

 

3.  Bwana Yesu anatufunulia utukufu wa Mungu.

 

Yohana anasema “Nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli”.  Katika kitabu cha Kutoka Biblia inatueleza utukufu wa Mungu ni nini.  Katika kitabu cha Kutoka 33:18-19 tunasoma hivi: “Mose akasema, 'Nakusihi unionyeshe utukufu wako.'  Mwenyezi-Mungu akamjibu 'Nitapita mbele yako na kukuonyesha wema wangu wote nikilitangaza jina langu, Mwenyezi-Mungu, Mimi nitamrehemu yule ninayependa kumrehemu na kumhurumia yule ninapenda kumhurumia.”  Tukiangalia kwa makini mistari ya sura ya 33, tunaona kwamba Mose alimwambia Mungu amwonyeshe utukufu wake.  Wakati Mungu anamjibu Mose, Mungu anamwambia mambo matatu:

 

(i) “Nitapitia mbele yako na kukuonyesha wema wangu.”

(ii) “Nitalitangaza jina langu, Mwenyezi-Mungu.”

(iii) “Nitamrehemu yule ninayependa kumrehemu, na kumhurumia yule ninayependa kumhurumia.”

 

Utukufu wa Mungu unajumlisha mambo haya matatu.

 

(i) Kwanza, utukufu wa Mungu unaonekana katika wema wake Mungu: “Nitapitia mbele yako na kukuonyesha wema wangu.”  Tunapaswa kuelewa kwamba wakati Biblia inatumia neno “wema,” siyo kama vile tunalielewa neno hili siku hizi.  Siku hizi tukiona mtu anasaidia watu tunasema kwamba huyo ni “Mtu mwema.”  Tukisikia kuhusu mtu ambaye aliishi sana Afrika na aliwajengea shule na hospitali watu maskini, utasikia watu wakisema kwamba “Huyo alikuwa mtu mwema, aliishi maisha mema.”  Mtu mwema kulingana na mawazo yetu ni yule amefanya matendo mazuri; ikiwa mtu amefanya matendo mazuri kama kuwasaidia maskini basi tunasema kwamba yeye ni mtu mwema.  Watu mara mingi hawako makini kutazama tabia za watu, bora tu mtu anatenda mambo mazuri.  Yule ambaye aliwajengea maskini shule na hospitali inawezekana ana tabia ya kumtusi na kumpiga bibi yake, ama mlevi na hata haamini Mungu.  Mara nyingi hatufikirii kuhusu mambo hayo bali tunaangalia matendo tu.

 

Wakati Biblia inasema “wema,” inamaanisha “utakatifu.”  Inamaanisha kuwa safi, kuwa kamilifu na bila dhambi kabisa.  Inamaanisha kuchukia dhambi na kutoroka dhambi.  Hii ndiyo sababu Yesu alisema, “Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu” (Marko 10:18).  Mungu ni mwema.  Hii inamaanisha kwamba Mungu ni mtakatifu; Mungu ni msafi na hana dhambi na anachukia dhambi kwa sababu yeye ni mtakatifu.  Utakatifu wa Mungu ulidhihirika mlimani Sinai wakati Mungu aliwapa Waisraeli sheria yake: “Palikuwa na ngurumo na umeme, na wingu zito juu ya mlima, na sauti ya baragumu iliyolia sana.  Watu wote waliokuwa kituoni wakatetemeka” (Kutoka19:16).  Yohana anatuambia kwamba Yesu Kristo alidhihirisha utakatifu wa Mungu (Yohana 1:14).  Katika utu na kazi ya Bwana Yesu tunaona vile Mungu anachukia dhambi.  Hii inaonekana wazi katika mahubiri ya Yesu dhidi ya dhambi hasa hasa katika kitabu cha Mathayo 23 ambapo analaani dhambi za Mafarisayo na Masadukayo.  Pia vile Mungu anachukia dhambi inaonekana zaidi wazi msalabani Kalivari.  Bwana Yesu Kristo alikufa msalabani kwa sababu Mungu ni mtakatifu na msafi na ni lazima ahukumu dhambi.  Yesu alikuja humu duniani kufanya kazi fulani: yaani kuwaokoa wateule wa Mungu kutoka kwa dhambi zao: “Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi” (1 Timotheo 1:15).  Njia moja tu Bwana Yesu angefanya hivi ni kuwalipia fidia watu wake kwa kufa msalabani.  Hii ndiyo njia tu ya pekee Mungu mtakatifu na mwenye haki angeweza kutosheka, na ndiyo njia tu ya pekee Mungu angetusamehe dhambi zetu.  Kifo cha Bwana Yesu kilikuwa dhihirisho ya utukufu wa Mungu: utukufu huu unadhihirisha kwamba Mungu ni mwema na mtakatifu, ni msafi na hana dhambi na anachukia dhambi na ni lazima aadhibu dhambi.

 

(ii) Pili, utukufu wa Mungu unadhihirika katika neema ya wokovu na huruma wa Mungu: “Nitalitangaza jina langu, Mwenyezi-Mungu.” Katika kitabu cha Kutoka, tunasoma kwamba Waisraeli walikuwa watumwa nchini Misri na wakamlilia Mungu awakomboe.  Kwa sababu hii Mungu akamtokea Musa kwa kijiti na akajiita “Bwana.”  Jina hili ambalo tunaita Yehovah, ni jina ambalo linahusika na agano ambalo Mungu kwa neema na huruma wake aliwakomboa Waisraeli kutoka Misri.  Ni jina ambalo Waisraeli walimwita wakati walipokuwa Misri, ni Mungu ambaye kwa neema na huruma wake aliyasikia maombi yao na kuwakomboa kwa mkono wake wenye nguvu.  Kwa hivyo Bwana Yesu Kristo anatuonyesha neema na huruma katika kazi yake ya wokovu.  Jina “Yesu” linamaanisha “Mungu ambaye anatuokoa.”  Kwa sababu alikuja hapa ulimwenguni na kutukomboa kutoka kwa nguvu za dhambi na mshahara wa dhambi zetu, ni dhihirisho la neema na huruma wa Mungu.  Kwa sababu alifunza kuhusu mfalme wa Mungu na kufa msalabani na akafufuliwa tena, haya yote yanaonyesha neema na huruma wa Mungu katika wokovu.  Hii ndiyo sababu Yohana anasema kwamba alikuwa amejawa na neema na ukweli.

 

(iii) Tatu, utukufu wa Mungu unaonekana katika nguvu za Mungu: “Nami nitamfadhili yeye nitakayemfadhali; nitamrehemu yeye nitakamrehemu.”  Utukufu wa kila kiongozi unapatikana katika nguvu ambazo ako nazo.  Katika ulimwengu wa siasa tunawaheshimu viongozi wa mataifa ambayo yako na mamlaka mengi ulimwenguni.  Mtu akisema kwamba yeye ni raisi wa nchi ndogo sana ambayo hatujawahi kusikia na awe hana usemi katika mambo ambayo inahusu ulimwengu, mtu huyu hatuwezi kumheshimu sana.  Lakini mtu ambaye ni kiongozi wa taifa kubwa katika ulimwengu ataheshimiwa sana.  Utukufu wa Mungu unaonekana katika nguvu na mamlaka ambayo ako nayo.  Nebukadreza ambaye alikuwa na mamlaka mengi alisema kuhusu Mungu, “Mamlaka yake ni mamlaka ya milele, na ufalme wake hudumu toka kizazi hata kizazi; na watu wote wanaonekana duniani wamehesabiwa kuwa si kitu, naye hufanya kama atakavyo, katika jeshi la mbinguni, na katika hao wanaokaa duniani; wala hapana awezaye kuuzuia mkono wake, wala kumwuliza, unafanya nini wewe?”(Danieli 4:34-35).

 

Maneno ambayo Mungu alimwongelesha Musa na maneno ambayo Nebukadreza aliandika yote yanaonyesha ukweli moja kumhusu Mungu: Mungu ni mwenye nguvu na mamlaka kwa jinsi anavyofanya na wanadamu na hawezi kuulizwa na yeyote anafanya nini: “Hapana awezaye kuuzuia mkono wake, wala kumwuliza, unafanya nini wewe?”  Utukufu huu wa nguvu na mamlaka unaonekana wazi katika kazi yake ya wokovu.  Ni jambo la kushangaza kwamba mara mingi watu hujiona kwamba wako na utawala katika wokovu.  Watu hawa wanapenda kuwaza kwamba ni hao wenyewe ambao waliamua kuokoka kwa kumkaribisha Yesu Kristo maishani mwao.  Pia kwamba ni hawa waliokuja kwa Kristo kwa kupenda kwao.

 

Lakini mawazo haya ni kinyume na mafunzo ya Biblia.  Biblia inatueleza kwamba, “Wokovu hutoka kwa Bwana” (Yona 2:9).  Biblia inatuambia kwamba kuna wengi ambao tangu kuumbwa kwa ulimwengu waliteuliwa kuwa vyombo vya utukufu; na kuna wengi ambao waliteuliwa kuwa vyombo vya uharibifu (Warumi 9:22-23).  Biblia inatueleza kwamba wale wote ambao wanapokea wokovu na msamaha wa dhambi zao wanafanya hivyo kwa sababu waliteuliwa na Mungu kabla ya kuumba ulimwengu kuwa waokoke (Waefeso 1:4:, 2 Wathesalonike 2:13-14); na kwamba wale wote ambao wanaangamia katika dhambi zao wanafanya hivyo kwa sababu wao ni vyombo vya uharibifu (Warumi 9:22; Yuda 4).  Hii haimaanishi ya kwamba wale ambao hawajaokoka wanaweza kumlaumu Mungu.  Ukweli ni kwamba walipenda dhambi zao na kubaki dhambini hadi kifo chao.

 

Kwa hivyo Yohana 1:14 inatufundisha mambo matatu ya muhimu kuhusu Yesu Kristo,  yaani Yesu alikuwa Mungu kamili na mwanadamu kamili; Yesu aliishi miongoni mwetu; na pia anatufunulia utukufu wa Mungu

 

Funzo la Tano: Tafadhali Soma Yohana 1:15-18.

 

1.  Bwana Yesu Kristo ndiye alitimiza unabii wote.

 

Tunasoma katika mstari wa 15, “Yohana alimshuhudia, akapaza sauti yake akasema, Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu.”  Yohana Mbatizaji alikuwa nabii kama manabii wote wa Agano la Kale. Katika mstari huu, tunasoma Yohana akisema kwamba Bwana Yesu alikuwako kabla yake.  Kwa ufupi Yohana Mbatizaji kile anasema hapa ni kwamba kama manabii wote katika Biblia, alikuwa anawaongoza watu kwa Yesu Kristo.  Wakati manabii wa Agano la Kale walipowahubiria watu wa Yudea na Waisraeli, ujumbe wao ulikuwa unamhusu Bwana Yesu Kristo.  Inaweza kuwa siyo rahisi kujua jambo hili katika vitabu vya unabii vya Agano la Kale.  Lakini ikiwa tutasoma vitabu hivi kwa uangalifu sana, tutaona kwamba kile manabii wanafanya ni kuonyesha kwamba sisi ambao ni watenda dhambi hatuwezi kutii Sheria ya Musa na kwamba njia tu tunaweza kuokolewa ni kupitia kwa huruma wa Mungu ndani ya Kristo Yesu.  Petro anasema,

 

 “Katika habari ya wokovu huo manabii walitafuta-tafuta na kuchunguza-chunguza, ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi.  Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo na utukufu utakaokuwako baada ya hayo. Wakafuniliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni.  Mambo hayo malaika wanatamani kuyachungulia” (1 Petro 1:10-12).

 

Katika mistari hii Petro anasema kwamba mahubiri ya manabii yalihusu neema ya Mungu ambayo ilikuwa ije kwa watu wake kupitia kwa kuteseka kwa Yesu Kristo na utukufu ambao ungefuata.  Hili ndilo lilikuwa kusudi kwa nini manabii wa Agano la Kale walitumwa.  Kwa hivyo Yohana Mbatizaji alisema, “Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu.”

 

2.  Bwana Yesu Kristo huwaletea watu wake baraka.

 

Yohana anasema, “Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema.”  Utimilifu wa neema yake inamaana kwamba Bwana Yesu amejawa na neema na kupitia kwa neema hii anawapatia watu wake baraka.  Kuna mambo mawili muhimu ambayo tunafunzwa hapa.

 

(i) Bwana Yesu Kristo ndiye hazina ya baraka za watu wake kutoka kwa Mungu.  Hazina ni mahali ambapo pesa za walipa ushuru zinawekwa, halafu serikali inaamua ni pesa ngapi itatumia kwa masomo, matibabu, na mambo mengine.  Hii ni afisi ya serikali ambayo wizara yoyote ikihitaji pesa inauliza.  Kwa njia hiyo hiyo, Bwana Yesu Kristo ndiye hazina ya baraka zote zinapatikana ambazo Mungu anataka kuwapatia watu wake.  Ni Kristo Yesu peke yake ambaye anaweza kutupatia baraka hizi.

 

(ii) Baraka hizi hazipatikani kwa sababu ya juhudi zetu, bali zinapeanwa bure kwa neema ya Kristo Yesu.  Sisi wenyewe hatuwezi kuamua ni baraka gani tunataka na baadaye kwa uwezo wetu tuzinunue.  Bali ni Bwana Yesu Kristo mwenyewe ambaye anaamua ni baraka gani zinatufaa kwa maisha yetu ya kiroho halafu anatupatia baraka hizi.  Lazima kila wakati tukumbuke kwamba Bwana Yesu Kristo anafanya kazi ya kutukamilisha.  Mambo mengi ambayo tunatamani yanaweza kuwa siyo mazuri na yakose kutusaidia katika kazi ya Bwana Yesu Kristo ya kutukamilisha.  Kwa hivyo ni Bwana Yesu Kristo mwenyewe ambaye anaamua ni baraka gani tunafaa kupokea na anatupatia baraka hizo.

 

3.  Bwana Yesu Kristo ndiye timizo la kila ahadi ambayo inapatikana katika Sheria ya Musa.

 

Yohana anasema kwamba, “Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.”  Jinsi tunavyoona katika mstari huu, Yohana anazungumza juu ya Sheria ya Musa na anailinganisha na kuja kwa Yesu Kristo: “Torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.”  Yohana anaposema hivi, anatukumbusha kwamba torati ya Musa ilipeanwa na sababu.  Kuna kuchanganyikiwa kwingi katika ulimwengu leo kuhusu torati ya Musa ikizingatiwa sana Sheria kumi.  Watu wengi wanawaza kwamba Mungu alipeana sheria hizi ili tuweze kujitahidi kwa kuzitii, na mwishowe wa maisha yetu kama tutakuwa tumejitahidi sana, tutapewa nafasi mbinguni.  Hivi ndivyo watu wanavyofikiria kuhusu sheria ya Musa ikizingatiwa sana Sheria kumi.

 

Ni muhimu sana kuangazia kwamba Biblia haisemi hivi kuhusu sheria hii.  Hakuna mahali popote katika Biblia ambapo panasema kwamba tukijitahidi sana kuwa waaminifu kwa Sheria Kumi na kuishi maisha mazuri na maisha ya kidini, basi tutapewa nafasi mbinguni.  Biblia haifunzi hivi kamwe.  Biblia inafunza kwamba ni mpango wa Mungu watu waokolewe kwa imani bali siyo kwa matendo.  Hivi ndivyo Ibrahimu alivyookolewa: “Akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki” (Mwanzo 15:6).  Paulo anawaelezea Wagalatia kwamba ikiwa Mungu amewatengenezea watu wake njia ya kuokoka, basi hawezi kubadilisha mawazo yake na kuweka njia nyingine tofauti.  Katika kitabu cha Wagalatia 3:8-18, mafunzo ya Paulo ni haya: “Ibrahimu hakuokolewa kwa sababu ya matendo yake mema au kutii Sheria ya Musa, bali aliokolewa kwa imani.  Wakati Mungu alimwokoa Ibrahimu kwa imani, alikuwa anatuonyesha kwamba hii ndiyo njia ya wokovu kwa kila mtu; siyo kwa matendo bali kwa imani.  Kwa hivyo wakati wa Ibrahimu Mungu alipanga njia ya jinsi watenda dhambi wanaweza kuokolewa.  Baada ya miaka 400 Mungu alimpa Musa Sheria Kumi.  Ni wazi kwamba njia ya kuokolewa siyo kupitia Sheria Kumi, kwa sababu Mungu tayari alikuwa amepanga jinsi watu wataokolewa.  Wakati Mungu alimpa Musa Sheria Kumi, hakuwa anasema kwamba watu wataokolewa kupitia kwa hizi sheria, kwa sababu alikuwa ameshapanga njia ya wokovu, yaani kwa imani pekee.”

 

Je, ni kwa nini Mungu alitupatia sheria?  Katika Wagalatia 3:19-25, Biblia inasema kwamba sheria ilipeanwa ili ituongoze kwa Kristo Yesu.  Kwa mfano, mtu ambaye anaishi mashambani ako na maumivu ya tumbo.  Halafu mmoja wa rafiki yake anamwambia kuhusu daktari ambaye anaweza kumshughulikia na ako katika hospitali moja mjini, lakini mtu huyu akataye ushauri huo.  Badala yake anajaribu kujitibu akitumia madawa ya kienyeji.  Lakini siku moja mwalimu anakuja katika kijiji hicho na kumfunza mtu huyu jinsi mwili wa mwanadamu unavyofanya kazi na aina ya ugonjwa ambao mtu huyo ako nao.  Baada ya mafunzo hayo mtu huyo anafahamu vyema kwamba ako na ugonjwa ambao unahitaji matibabu kwa haraka; kwa hivyo anaenda kwa daktari.  Hivi ndivyo sheria inavyofanya kazi.  Sheria inatuonyesha kwamba tuko na ugonjwa hatari sana ambao ni dhambi na tiba yake ni kuenda kwa Yesu Kristo ili atuokoe, hakuna chochote tunaweza kufanya.

 

Kwa hivyo tumeona kwamba kuna uhusiano mkubwa sana kati ya Musa na Bwana Yesu Kristo; Musa alitengeneza njia kwa Yesu Kristo.  Sheria inatuonyesha dhambi zetu na pia kwamba hatuwezi kufanya lolote kujiokoa isipokuwa kuenda kwa Yesu Kristo.  “Torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.”

 

4.  Bwana Yesu Kristo anatuonyesha Mungu Baba ni nani.

 

Yohana anaandika, “Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.”  Tuko hapa na kumbusho kwamba moja wapo ya sababu ya Bwana Yesu Kristo kuja hapa ulimwenguni ni kutuonyesha Mungu Baba ni nani.  Tangu kuanguka kwa Adamu na Hawa, tulipoteza ushirika na Mungu.  Tunazaliwa katika ulimwengu huu tukiwa watenda dhambi na maadui wa Mungu.  Hatumjui Mungu anafanana aje.  Kuna wengi katika ulimwengu ambao wamedanganywa na dhambi na wanafikiria kwamba wanamjua Mungu.  Wanasema mambo kama haya, “Ukiishi maisha mazuri na kujitolea kwa kazi ya Mungu, basi Mungu atakubariki na atakupa nafasi mbiguni kama zawadi ya juhudi zako.”  Kuna wahubiri wengi leo ambao wanahubiri mambo kumhusu Mungu ambayo ni ya uongo.  Ukweli ni kwamba kwa sababu tumezaliwa kwa dhambi, sisi ni maadui wa Mungu na hatumjui Mungu.

 

Kwa hivyo Bwana Yesu Kristo alikuja ulimwenguni ili atuonyeshe Mungu Baba ni nani.  Alikuja kutuonyesha kwamba Mungu ni mtakatifu na kwamba anachukia dhambi na chuki takatifu.  Alikuja kutuonyesha kwamba Mungu amejawa na upendo, neema na huruma.  Alikuja kutuonyesha kwamba Mungu anawajali watu wa ulimwengu; anajawa na huruma wakati anapowaona wakiteseka na anajawa na furaha wakati anapowaona wako na imani ndani mwake.  Alikuja kutuonyesha kwamba Mungu ni mwenye nguvu na ako na uwezo wa kuwatosheleza na kuwalinda watu wake.  Alikuja pia kutuonyesha kwamba Mungu ni Mungu wa wokovu ambaye hawaachi watu wake katika dhambi zao bali anawaokoa kwa mkono wake wenye nguvu.  Mambo haya yote yanaonekana katika kazi yake Kristo Yesu na yote yamepangwa kutuonyesha jinsi Mungu Baba alivyo.

Masomo kutoka kwa Waebrania 1:1-3

 

Kifungu hiki, kama Yohana 1:1-18 kimejaa mafunzo mengi kuhusu bwana Yesu Kristo

 

Funzo La Sita, Tafadhali Soma Kitabu cha Waebrania 1:1-3.

 

Katika kifungu hiki, mwandishi anatueleza kwamba Mungu ameongea nasi watu wake kupitia mwanawe Yesu Kristo.  Msitari wa 2 mwandishi anatueleza mambo mengi kuhusu Bwana Yesu.

 

1.  Bwana Yesu Kristo ndiye mrithi wa yote.

 

Mwandishi wa Waebrania anasema “Aliyemweka kuwa mrithi wa yote.”  Hii inamaanisha kwamba Bwana Yesu Kristo amekusudiwa na Mungu kuwa yeye ndiye atakayerejesha dunia hii katika hali yake ya utukufu wa mwanzo.  Katika kitabu cha Mwanzo tunaambiwa kwamba Mungu aliumba kila kitu na kilikuwa kizuri.  Lakini wakati Adamu alianguka dhambini, Mungu alitangaza laana juu ya dunia.  Kabla ya kuanguka dhambini Adamu na Hawa walikuwa na amani na kila kitu ambacho Mungu alikuwa ameumba.  Shamba lile Mungu alikuwa ametengeneza halikuwa linazaa miiba na michongoma, na pia hakukuwa na kiangazi wala mafuriko.  Kila kitu kilichoumbwa kilikuwa kizuri na kazi ya mwanadamu shambani ilikuwa ya kufurahia sana.  Lakini baada ya Adamu kuanguka dhambini, ulimwengu hukuwa wa kufurahia tena, kwa sababu ya laana.  Miiba na michongoma zikaanza kumea, na mwanadamu akawa ni lazima ale kupitia jasho lake.  Hii haimaanishi kwamba Mungu aliamua kuangamiza ulimwengu wote milele.  Kuna watu leo ambao wanaamini kwamba wakati Yesu atarudi ulimwengu huu utaangamizwa kabisa na wale wameokoka watenda pahali panaitwa mbinguni.  Tafadhali usishangae kuelezwa kwamba huu si ukweli.  Si ukweli kwamba wakati Yesu atakaporudi humu duniani, ataangamiza dunia yote milele na wale wameokoka wataenda pahali panaitwa mbinguni.

 

Biblia inaeleza wazi kwamba Mungu anaendelea na kuurejesha ulimwengu katika hali ya utukufu wa hapo mwanzoni.  Mungu anaendelea kuondoa hali ya laana kutoka duniani ndipo wakati Kristo atakaporudi ataurejesha ulimwengu huu katika hali yake ya mwanzo.  Biblia inasema, “Kwa kuwa viumbe vyote vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu” (Warumi 8:18-21).  Kazi hii ya kurejesha ulimwengu katika hali uliokuwa imepewa Bwana Yesu Kristo.  Hii ndiyo sababu Biblia inasema kwamba ni mapenzi ya Mungu, “Kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia.  Naam, katika yeye huyo” (Waefeso 1:10).  Kwa hivyo wakati Biblia inasema kwamba Yesu ndiye mrithi wa vyote, inamaanisha kwamba yeye ndiye kiongozi wa mambo yote hapa ulimwenguni na pia mbinguni na kwamba yeye ndiye atakayekamilisha mpango mkubwa wa Mungu wa wokovu wa wateule wake na pia kuurejesha ulimwengu katika hali ya mwanzoni.

2.  Bwana Yesu Kristo ni Mungu.

 

Tayari tumezungumzia jambo hili katika sura ya kwanza ya kitabu cha Yohana.  Ingawa hivyo tunapaswa kukumbuka kwamba Agano Jipya linazungumzia jambo hili mara mingi.  Si Yohana pekee anatueleza kwamba Bwana Yesu Kristo ni Mungu.  Mwandishi wa Waebrania pia anaeleza jambo hili kwa njia mbili.

 

(i) Kwanza, mwandishi wa Waebrania anatuambia kwamba Bwana Yesu Kristo ndiye muumba wa ulimwengu.  Anasema, “vyote vilifanyika kwa huyo.”  Hii ni sawa na vile Yohana anasema: “vyote vilifanyika kwake huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika” (Yohana 1:3).

 

(ii) Pili, Mwandishi wa Waebrania anasema, “Yesu ndiye mng'ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake.”  Hii inamaanisha kwamba Bwana Yesu Kristo anatudhihirishia utukufu na jinsi Mungu alivyo.  Kristo ndiye mwanga wa utukufu wa Mungu kwa hivyo ndani yake tunaona vile Mungu ako.  Kristo ndiye mwakilishi wa Mungu na anamwakilisha Mungu katika kila jambo.  Ni kwa njia moja tu ambayo Yesu anaweza kufanya mambo haya yote, ni lazima awe Mungu.

 

3.  Bwana Yesu Kristo anatawala vitu vyote kwa neno lake lenye nguvu.

 

Kutawala inamaanisha kuendelesha.  Mwandishi wa Waebrania anatueleza hapa kwamba Bwana Yesu Kristo ndiye aliuumba ulimwengu, na pia ndiye anauongoza.  Yesu anatumia neno lake kutawala ulimwengu.  Kwa hivyo Yesu Kristo aliumba ulimwengu kwa neno lake lenye nguvu na anautawala kwa neno lake.  Kuna mambo mawili ambayo tunaelezwa hapa.

 

(i) Kwanza tunaambiwa kwamba maisha yetu yako mikononi mwa Kristo.  Bwana Yesu Kristo anatupatia hewa ya kupumua, jua na chakula kila siku.  Haya mambo yote Yesu huamrisha yafanyike, yaani anaamrisha jua liwake na anaamrisha mvua inyeshe.  Kristo anaamrisha mimea ikue ili tupate chakula.  Mambo haya yote yanafanyika kwa sababu Kristo anatawala ulimwengu kwa neno lake lenye nguvu.

 

(ii) Pili tunaelezwa kwamba mambo yote ambayo yanayofanyika humu duniani yanatawaliwa na Kristo.  Ni Kristo pekee ambaye aliuumba ulimwengu na ni yeye pekee anatawala.  Kuna watu wengi ambao wanaamini kwamba shetani ana nguvu nyingi kama Mungu na kwamba shetani anaweza kufanya mambo ambayo Mungu hataki yafanyike.  Wanaamini kwamba shetani anaweza kusababisha ajali ama anaweza kuleta magonjwa hata ikiwa Mungu hataki mambo hayo yatendeke.  Biblia haifundishi mambo hayo.  Biblia inafundisha kwamba Bwana Yesu Kristo anatawala ulimwengu wote kwa neno lake lenye nguvu.  Ni Kristo ambaye anaamrisha wala si shetani.  Ni Kristo ambaye ako na mamlaka na nguvu zote wala siyo shetani.

 

Funzo La Saba: Tafadhali Soma Waebrania 1:3.

 

Katika funzo hili, tutatazama sehemu nyingine ya mstari huu ambayo inasema kwamba, “Akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu.”  Kuna mafunzo mawili muhimu sana ambayo tunasoma kutoka kwa kifungu hiki.

 

1.  Bwana Yesu Kristo amekamilisha kazi yake ya kufanya utakaso wa dhambi za watu wake.

 

Mwandishi wa Waebrania anasema kwamba, “Akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu.”  Katika mstari huu ni wazi kwamba Bwana Yesu Kristo amemaliza kazi yake ya kufanya utakaso wa dhambi za watu wake.  Biblia inasema kwamba, “Akiisha kufanya utakaso,” kumaanisha kwamba kazi ilikamilika, pia inasema kwamba “Aliketi mkono wa kuume.”  Kwa kawaida mtu huketi chini baada ya kumaliza kazi zake.  Bwana Yesu Kristo amemaliza kazi yake ya kuwafanyia utakaso wa dhambi watu wake.  Hii inamaanisha kwamba njia moja tu mtu anaweza kuoshwa dhambi zake ni kupitia kwa damu ya Yesu Kristo.  Hili ni jambo ambalo Biblia inafunza kwa wazi sana.  Biblia inasema kwamba, “Na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote” (1 Yohana 1:7).

 

Kuna watu leo katika nchi yetu ambao huwaza kwamba tunaoshwa kutoka kwa dhambi zetu na maji ya ubatizo.  Wanaamini kwamba mtu akitaka kuoshwa dhambi zake na kuokolewa, basi ni lazima abatizwe kwa maji.  Lakini hakuna mahali popote ambapo Biblia inafunza jambo hili.  Biblia ni wazi kwamba ni damu ya Yesu Kristo pekee ambayo inaweza kutuosha kutoka kwa dhambi zetu.  Mtu anaweza kubatizwa mara mia, lakini ikiwa mtu huyo hajawahi kutubu dhambi zake na kumwamini Kristo Yesu, basi ubatizo haumfaidi chochote: bado mtu huyo ako katika dhambi zake na yeye ni muovu machoni pa Mungu.  Bwana Yesu Kristo ni Yeye tu ambaye amepeana utakaso wa dhambi, siyo maji ya ubatizo.

 

2.  Bwana wetu Yesu Kristo ndiye Kuhani Mkuu.

 

Bwana Yesu Kristo amekalia mkono wa kulia wa Mungu Baba akiwa kuhani Mkuu wa watu wake.  Kuna mambo mawili ambayo Bwana Yesu Kristo anafanya akiwa Kuhani mkuu wa watu wake.

 

(i) Anatuombea.  Ni jambo la kutufariji kwamba Bwana Yesu Kristo anawaombea watu wake kila siku.  Anaombea sana hali yetu ya kiroho, ili tuweze kukua katika ukristo wetu na kuendelea kuwa watakatifu ili kila siku tuendelee kuwa katika mfano wake.

 

(ii) Anafanya maombi yetu na kazi zetu zikubalike mbele ya Mungu.  Maisha ya ukristo ni maisha ya imani siyo matendo mazuri.  Hatuwezi kusema kwamba Mungu atakubali maombi yetu na kazi zetu kwa sababu tumekuwa watu wazuri.  Ni kwa imani tu ndiyo maombi yetu yanakubalika mbele ya Mungu kwa sababu Yesu Kristo Kuhani wetu Mkuu anayafanya yakubalike.

 

3.  Bwana Yesu Kristo pekee ndiye Bwana wa kanisa lake.

 

Mwandishi wa Waebrania anasema kwamba, “Aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu.”  Maneno “Ukuu wa huko juu” yanamaanisha kwamba Mfalme aliye huko mbinguni.  Mwandishi anatueleza kwamba Bwana Yesu Kristo ndiye aliye na mamlaka kamili mbinguni na ulimwenguni hata katika kanisa lake.  Hii ndiyo sababu Paulo anasema, “Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote” (Wakolosai 1:18).

 

Kuna kuchanganyikiwa kwingi kuhusu jambo hili nchini mwetu leo.  Ukimwuliza mtu, “Nani ndiye kichwa cha kanisa?” mara mingi atasema kwamba, “Ni mchungaji au askofu.”  Hii ni kwa sababu haelewi ni nini Biblia inafunza na yale amefunzwa ni uongo mtupu.  Kuna wachungaji wengi na maaskofu ambao husema kwamba, “Mimi ndimi kichwa cha kanisa hili na ni lazima mnifuate na kutii yale ambayo ninasema.”  Kwa kusema haya wamepotea kabisa.  Hakuna mahali popote katika Biblia ambapo tunaambiwa kwamba mchungaji au askofu ndiye kichwa cha kanisa.

 

Tunaambiwa wazi kabisa kwamba Bwana Yesu Kristo ndiye kichwa cha kanisa. Ni Yeye tu ambaye tunafaa kusikiliza na ni Yeye pekee ambaye tunafaa kutii.  Ikiwa mchungaji au askofu atasema mambo ambayo yako kinyume na neno la Mungu au kuwauliza watu wafanye yale ambayo ni kinyume na neno la Mungu, basi watu hawafai kumsikiliza na kumtii mchungaji au askofu huyo.  Kutii mchungaji huyo ni dhambi kwani kwa kumtii wanamfanya kuwa kichwa cha kanisa na siyo Bwana Yesu Kristo.  Siku moja wachungaji hawa wataeleza vile walifanya kazi ambayo Bwana aliwapa.

 

 

Masomo Kutoka Kitabu cha Wafilipi 2:2-8.

 

Kifungu hiki, kama zile mbili ambazo tumesoma, kiko na mafundisho muhimu kuhusu Bwana Yesu Kristo.

 

Funzo La Nane, Tafadhali Soma Wafilipi 2:3-8.

 

Katika kifungu hiki tunapata mafundisho yafuatayo.

 

1.  Hatupaswi kutenda lolote ili tujifaidi wenyewe.

 

Paulo anasema katika msitari wa 3, “Msitende neno lolote kwa kushindana wala majivuno.”  Sisi wanadamu, kwa sababu ya dhambi ya Adamu, tunazaliwa tukiwa watu wachoyo.  Tunashughulikia tu mambo yetu wenyewe pekee na hatujali mambo ya wengine.  Tunafikiria tu vile tutapata pesa na vile tutaishi maisha mazuri hata ikiwa inatulazimu kuwandanganya wenzetu na kuwaibia.  Bora tu tunaishi maisha ya furaha huku duniani ni wazi kwamba hatujali mambo ya wengine.  Lakini wakati tunaokoka tunakuwa na mabadiliko.  Wale ambao wameokoka hawaishi kama watu wa dunia.  Hawakimbizani na anasa na mali za dunia.  Wale ambao wameokoka hawafanyi mambo ya kujifaidi kibinafsi bali wanawaona wengine kuwa bora kuliko wao.  Hii inamaanisha wanashughulikia wengine kwanza: “Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine” (msitari wa 4).

 

Hili ni jambo ambalo siyo rahisi kwetu, Tumezaliwa tukiwa tumekufa kwa dhambi na kuishi kwa dhambi kwa muda mwingi.  Hii inamaanisha kwa miaka mingi tumeishi maisha ya uchoyo na kujifikiria sisi wenyewe na mahitaji yetu.  Hatukushughulikia wengine na mahitaji yao ila sisi wenyewe.  Chochote tulikuwa tukifanya kilikuwa ni cha kujinufaisha na kutengeneza maisha yetu wenyewe.  Kwa hivyo ni vigumu sana kugeuka kwa haraka kutoka kwa hali hii.  Yaani kuacha kujifikiria sisi wenyewe na kuanza maisha ya kujali wengine kwanza.  Haya siyo mambo rahisi kuanza lakini Biblia inatuamrisha kufanya hivyo.

 

2.  Yesu Kristo ndiye mfano mkuu katika jambo hili.

 

Paulo anaendelea kusema katika kifungu hiki, “Iweni na nia hiyo hiyo ndani yenu ambayo pia ilikuwa ndani ya Kristo Yesu.”  Paulo anasema kwamba tunapaswa kuangalia mfano mkuu kutoka kwa Yesu ikiwa tutatii amri hii ya kuwaona wengine kuwa bora zaidi ya sisi.  Tunapaswa kukumbuka hivi ndivyo Yesu Kristo alifanya.  Yesu alikuja ulimwenguni siyo kwa sababu ya mahitaji yake bali yetu.  Yesu alikuja kwa sababu tulikuwa tumekufa dhambini na hatungeweza kujiokoa kwa uwezo wetu.  Yesu hakujali kuhusu starehe zake na mahitaji yake.  Yesu kuja duniani ilikuwa jambo la uchungu sana, watu walimkataa, wakamtesa na mwishowe wakamwua.  Yesu alijua hivi ndivyo mambo yatakuwa atakapokuja duniani lakini alijali mahitaji ya wengine kwanza ndipo akaja.  Yesu alikuja kuwaokoa watu wake kutoka kwa dhambi zao.  Kwa hivyo Yesu ndiye mfano mkuu wa kuonyesha vile tunapaswa kujali maslahi ya wengine kwanza.

 

3.  Bwana Yesu Kristo alijinyenyekeza kwa ajili ya watu wake.

 

Paulo anaendelea kusema katika kifungu hiki kwamba Bwana Yesu Kristo, “Ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena alipooneka ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam mauti ya msalaba!”  Kile Paulo anasema hapa ni kwamba Yesu Kristo ni Mungu kamili, lakini hakutumia mamlaka yake, cheo chake na haki zake, bali “alijinyenyekeza.”  Paulo hasemi Yesu Kristo aliacha kuwa Mungu wakati alikuja duniani bali anasema Yesu alijinyenyekeza akiwa Mungu na hakutumia haki zake kwa ajili ya watu wake.

 

Labda mfano huu utatusaidia kuelewa jambo hili zaidi.  Hebu fikiria kuhusu mfalme mwenye mamlaka kubwa anasikia kuna kijiji fulani katika sehemu yake ya ufalme ambapo watu wako na jaa  na magonjwa sana, halafu anaamua kwenda kujionea mwenyewe vile hali iko na jinsi anaweza kusaidia.  Mfalme huyu anajua akienda uko akiwa amevaa mavazi yake ya serikali hataweza kujua mambo mengi, kwa sababu watu wa kijiji hicho wakisikia mfalme anakuja watavaa nguo mzuri ili wamkaribishe.  Mfalme akifanya hivi ataweza tu kuongea na wale wako katika mamlaka na wale wanaheshimika sana huko kijijini na hatapata nafasi ya kuongea na mwananchi wa kawaida ili amweleze shida ako nazo.

 

Basi mfalme huyu anaamua kutembelea kijiji hicho akiwa amevaa mavazi ya kawaida, anavaa mavazi ya mtu wa kawaida halafu anaenda kijijini.  Mfalme akiwa katika hali hiyo itakuwa rahisi kuwatembelea watu katika nyumba zao na kuongea nao kuhusu matatizo yao na jinsi serikali inaweza kuwasaidia.  Kufanya jambo hili haimaanishi kwamba mfalme amejiuzulu, bali ametumia haki alizo nazo kuwafikia wananchi hawa.  Amechagua kuja huku kijijini bila msafara wake na bila wanajeshi wake lakini angali yeye ndiye mfalme wa nchi hiyo.

 

Vivyo hivyo Bwana Yesu Kristo hakujiuzulu kuwa Mungu wakati alikuja duniani.  Yesu alikuwa Mungu na ataendelea kuwa Mungu milele.  Lakini wakati alikuja duniani aliamua hatatumia haki zake alizo nazo.  “Bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa.”  Huu ndiyo mfano sisi watumishi wa Mungu tunapaswa kufuata.  Ikiwa ndani ya kanisa watu wataanza kutilia mkazo sana kuhusu haki zao na kuanza kufikiria kuwa wao ni watu wakubwa na wa maana sana kuliko wengine kutatokea migawanyiko katika kanisa hilo.  Lakini ikiwa kila mtu kanisani, hata mchungaji, atajinyenyekeza na kufuata mfano wa Kristo kutakuwa na umoja katika kanisa hilo.

 

 

 

Funzo La Tisa, Tafadhali Soma Wafilipi 2:9-11.

 

Katika Wafilipi 2:3-8 tuliona vile Kristo alikuja duniani na kuwa mtumishi.  Yaani Kristo Yesu alijinyenyekeza.  Paulo anasema kwamba kwa sababu Kristo alijinyenyekeza, Mungu alimwinua sana.  Kuna mambo mawili tunapata katika kifungu hiki.

 

1.  Bwana Yesu Kristo ndiye ako na cheo cha juu sana na amepewa jina lililo zaidi ya majina yote.

 

Paulo anasema katika msitari wa 9, “Kwa hivyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia jina lile lipitalo kila jina.”  Wakati Yesu alipaa mbinguni baada ya kufa na kufufuka, alikaa upande wa kuume wa Mungu Baba.  Hii ni kwa sababu mamlaka yote mbinguni na duniani amepewa yeye (Mathayo 28:18).  Biblia inasema kwamba Bwana Yesu Kristo ako na mamlaka yote na uwezo wote.  Ni yeye tu pekee ako na uwezo huu.  Hakuna mwanadamu yeyote, ama malaika, au shetani ambaye ako na mamlaka na uwezo kama Yesu.  Shetani hayuko kiwango moja na Yesu.  Yesu amepewa kiti cha enzi na jina kuu kuliko majina yote.  Hii inamaanisha:

 

(i) Kristo ako na uwezo na nguvu kwa mambo yote hapa ulimwenguni.  Hakuna chochote kinachofanyika hapa duniani ambacho kinamzidi nguvu.  Tunaishi ulimwenguni, mahali ambapo mambo mengi hutendeka kama mitetemeko ya ardhi, njaa na ajali zinazofanyika kila wakati.  Tunasoma juu ya matokeo haya katika nchi yetu na nchi zingine za dunia, na wakati mwingine tunaweza kufikiria kwamba shetani ako na nguvu za kutenda mambo haya ambayo Mungu hawezi kuzuia.  Tunaweza kufikiria kwamba shetani anafanya vitu ambavyo Mungu hakutaka vifanyike.  Lakini mafikira haya hayaambatani na mafunzo ya Biblia.  Mungu ndiye anaongoza kila jambo na Mungu anathibiti kila kitu mikononi mwake.  Ni Yesu ambaye amepewa cheo cha juu sana, si shetani.  Katika Agano la Kale, tunasoma ya kwamba wakati shetani alitaka kumletea Ayubu majaribu, alipata ruhusa kutoka kwa Mungu kwanza.  Hangemguza Ayubu kama Mungu hangemruhusu.  Na pia shetani angemfanyia tu Ayubu kile Mungu alikuwa amemkubalia kufanya.  Hangemwua Ayubu kwa sababu hakuwa amepewa ruhusa.  Mungu ndiye anaongoza kila kitu, na Yesu ndiye aliye katika kiti cha enzi.  Hatuwezi kuelewa njia zake kila wakati lakini ni lazima tukubali kwamba yeye ndiye mfalme wa milele ambaye anaongoza ulimwengu wote.  Hatuwezi kuelewa ni kwa nini ajali hutendeka na ni kwa nini mitetemeko ya ardhi hutokea na hata njaa, na pia hatuwezi kuelewa ni kwa nini magonjwa huja kwa watu fulani.  Haya ni mambo hatuwezi kuyaelewa, lakini ni lazima tuamini ya kwamba shetani hawezi kufanya jambo lolote ambalo Mungu hataki.  Mungu ndiye anayeongoza ulimwengu wote.

 

(ii) Yesu ako na mamlaka kwa mambo yote katika kila nchi ulimwenguni.  Yeye ndiye anayekalia kiti cha enzi na amepewa jina lenye uwezo na nguvu kuliko majina yote.  Biblia inaeleza wazi kwamba Mungu ndiye anaongoza siasa za nchi mbalimbali na ni yeye anayechagua viongozi wa nchi mbalimbali.  Hivi ndivyo Biblia inasema, “Kila mtu aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu.  Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu” (Warumi 13:1-2).  Angalia kwa makini kile Biblia inasema hapa.  Biblia inasema hakuna uongozi ambao hujawekwa na Mungu: Mungu ndiye anaweka kila uongozi hapa dunia.  Na pia hii inaweza kutushangaza.  Inawezekanaje Yesu Kristo kuchagua uongozi katika nchi za waislamu kama nchi ya Usaudia na Afghanistani?  Inawezekanaje kwamba Mungu achague viongozi wa nchi hizo ilihali nchi hizo na watu wake ni maadui wa Mungu na kanisa lake?  Haya ni mambo hatuwezi kuelewa, lakini haifai kuamini kwamba kuna mambo hutendeka bila uongozi wa Mungu.  Hakuna kitu kinashida nguvu za Mungu.  Katika Agano la Kale, Mungu ndiye aliyemwinua mfalme Nebukadreza kutawala Yerusalemu na kuwapeleka watu wa Yuda katika utumwa.  Hakuna kitu kinashinda nguvu za Mungu.

 

(iii) Yesu Kristo pekee ndiye aliye na mamlaka juu ya kanisa lake.  Tunapoangalia katika kanisa tunawaona watu wanaoonekana kuwa na nguvu na mamlaka.  Kwa kawaida kanisa huwa na wazee ambao wamechaguliwa kuwa viongozi, na katika makanisa mengine mtu mmoja huchaguliwa ambaye ni mchungaji.  Pia kanisa inaweza kuwa na askofu na kadhalika.  Kwa watu wengi hii inaweza kuonekana kwamba wazee viongozi, wachungaji na maaskofu wako na mamlaka na nguvu zote, hata wakati mwingine mtu anaweza kufikiria kwamba yeye ako na mamlaka kwa sababu yeye ni askofu au mchungaji.  Lakini hii siyo kweli.  Bwana Yesu Kristo ndiye mchungaji mkuu, yeye ndiye kiongozi mkuu wa kanisa, yeye ndiye Bwana wa kanisa, yeye ndiye anayeongoza mambo yote kanisani.

 

Ukweli huu ni wa kuwafariji wakristo wote.  Maisha yetu ya kiroho hayako mikononi mwa watu wengine.  Si kweli kwamba maisha yetu ya kiroho yamo mikononi mwa wachungaji na maaskofu.  Hawa watu ni wafanyakazi wa Mungu na wameinuliwa kuwatumikia watu wa Mungu.  Kwa hivyo kila mtu ambaye ameokoka anaweza kufurahishwa na ukweli huu, kwamba Yesu Kristo ndiye kiongozi wetu.

 

Ukweli huu pia unaleta mambo ya kufikiria sana kwa wale ambao ni viongozi wa makanisa.  Ni rahisi sana kwa mtu ambaye ni mchungaji au askofu kufikiria kwamba yeye ndiye anaongoza.  Pia mtu anayeongoza anaweza kujaribiwa na kuanza kutumia cheo chake vibaya.  Mtu kama huyu anaweza kuwa na mamlaka juu ya matumizi ya pesa kanisani na aanze kuchukua pesa kwa matumizi yake ya kibinafsi bila kuwaeleza washirika wenzake.  Ni rahisi sana kwa watu hawa kufikiria kwamba hakuna anayejua kile wanachofanya kama vile kuchukua pesa kwa siri.  Hii si kweli.  Bwana Yesu Kristo ndiye kiongozi wa kanisa na anajua chochote tunachotenda hata kwa siri.  Hatuwezi kufanya chochote bila yeye kujua.  Yesu alipokuwa hapa duniani, mmoja wa wanafunzi wake aliyeitwa Yuda Iskarioti aliiba pesa.  Yesu Kristo alijua kwamba Yuda anaiba pesa kila mara lakini hakusema chochote, na Yuda alidhani kwamba hakuna anayejua matendo yake.  Hivi ndivyo Kristo anafanya mambo.  Yesu Kristo ako na hekima na kwa hivyo anafanya mambo yake kwa hekima.  Mtu ambaye ako na cheo cha mamlaka kanisani anaweza kutumia cheo hiki vibaya kwa manufaa yake mwenyewe.  Yesu Kristo hatasema chochote kwa mtu huyu lakini hii haimaanishi kwamba anapuuza mambo haya.  Ilipofika wakati wa hukumu Yuda Iskarioti alihukumiwa na kutupwa jahanamu.

 

2.  Kila goti litapigwa chini na kila ulimi utakiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana.

 

Paulo anasema katika Wafilipi 2:10-11, “Ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi, na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana kwa utukufu wa Mungu Baba.”  Wakati tunasoma kifungu hiki tunaweza kufikiria kwamba haya ni mambo yatakayotendeka wakati Yesu atakaporudi.  Tunaweza kufikiria kwamba wakati Yesu atarudi ulimwenguni ndipo kila goti litapigwa na kila ulimi kukiri Yesu ni Bwana, lakini kabla ya hayo, watu wengi duniani hawatakiri kwamba Yesu ni Bwana.  Hivi ndivyo tunaweza kufikiria kuhusu mistari hii.  Lakini hii si kweli.  Paulo haandiki kuhusu mambo yanayokuja bali anaongea kuhusu mambo yanayofanyika wakati huu.  Biblia inafundisha kwamba kuna watu wa aina mbili hapa duniani:

 

(i) Kuna wale ambao ni wafanyikazi wa Yesu Kristo na wanapiga magoti na kukiri kuwa Yesu ni Bwana kwa furaha.  Hili ni kundi la wale wote ambao wameokoka.  Kama mtu ameokolewa kupitia kwa damu ya Yesu Kristo basi yeye ni mtumishi wa Yesu.  Hata kama anafanya kazi kwa afisi mjini ama ni mkulima mashambani yeye ni mtumishi wa Yesu.  Jukumu lake kuu ni kumtumikia Yesu na kumletea utukufu.  Hawa ndiyo watu wanaopiga magoti na kukiri kwa vinywa vyao kwamba Yesu ni Bwana.

 

(ii) Kuna wale ambao hawajaokoka lakini hufanya mapenzi ya Mungu bila wenyewe kujua.  Hiki ni kikundi cha wale wote ambao hawajaokoka.  Hawa hawana haja na Kristo na kumtumikia.  Hamu yao kuu ni kupata vitu vya dunia na kufurahia anasa za dunia, na hawajali mambo ya Yesu.  Lakini Mungu anaongoza maisha yao ingawa hawajui na hawakubaliani na haya.  Ni Mungu anayeamua mahali watazaliwa, mahali pa kusoma, kiwango cha elimu watakachopata, kazi watayofanya, yule watakayeoa na kadhalika.  Yaani Mungu anaongoza maisha ya kila mtu hapa ulimwenguni, na pia Mungu hutumia kila mwanadamu duniani kwa mapenzi yake.  Wale ambao hawajaokoka hawatambui hili lakini Mungu huwatumia kwa mapenzi yake mwenyewe.  Kuna mifano miwili katika Biblia ambayo inaonyesha mambo haya waziwazi.

 

Kwanza, katika kitabu cha Isaya 45:1, Mungu anaongea kuhusu mfalme wa Uajemi aliyeitwa Koreshi na anasema, “Haya ndiyo Bwana amwambiayo Koreshi masihi wake, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume, ili kutiisha mataifa mbele yake, nami nitalegeza viuno vya wafalme.”  Sasa Koreshi hakuwa Myahudi bali alikuwa Muajemi.  Zaidi ya haya hakuwa ameokoka, alikuwa akiabudu miungu.  Ni wazi kwamba alijua machache kuhusu Mungu mmoja anayeishi.  Lakini Mungu alimtumia kutimiza mapenzi yake ya kuwarudisha Wayahudi nyumbani kwao.  Hii ndiyo sababu Koreshi anaitwa mwenye kupakwa mafuta na Mungu.  Koreshi alifanya mapenzi ya Mungu bila kujua.  Kulingana na mafikira yake, Koreshi alifanya yale yaliyokuwa ya manufaa kwa nchi yake.  Mungu alisema kuhusu Koreshi, “Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa.”

 

Pili, katika kitabu cha Matendo ya Mitume, tunasoma kwamba kanisa la kwanza lilipoomba wakati lilipitia mateso, walisema, “Maana ni kweli Herode na Pontio Pilato pamoja na mataifa na watu wa Uisraeli, walikusanyika katika mji huu juu ya mtumishi wako mtakatifu Yesu, aliyemtia mafuta.  Ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee” (Matendo ya Mitume 4:27-28).  Wakristo katika kitabu cha Matendo ya Mitume walielewa kwamba ulimwengu mzima uko chini ya uongozi wa Mungu, na hata wale ambao hawajaokoka hutimiza mapenzi ya Mungu bila wao kujua.  Hii ndiyo sababu walisema kwenye maombi yao kwamba wakati Herode, Pontio Pilato, mataifa na watu wa Uisraeli walikusanyika katika mji wa Yerusalemu na kupanga kumwua Yesu walikuwa wanatekeleza mapenzi ya Mungu.  Bila kujua walikuwa wamekwisha piga magoti chini kupitia kwa matendo yao na kukiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana na kwamba yeye anaongoza maisha ya kila mmoja na anatumia kila mmoja kwa utukufu wake na mapenzi yake.