“Inapaswa kumgeukia Mungu kwa
kutubu dhambi na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo” (Matendo 20:21).
“Je, ninahitaji kufanya nini
ili niokoke?” Pengine wewe umejiuliza
swali hili mara mingi. Unajua kwamba
hujaokoka. Unajua kwamba bado uko ndani
ya dhambi zako na unajua kwamba ukifa katika hali hii basi bila shaka utatupwa
jahanum. Unajua kwamba Mungu ni
mtakatifu na mwenye haki na ukiendelea kukaa katika hali hii, Yeye hatakuruhusu
kuingia mbinguni. Je, ni nini unahitaji
kufanya ili uokoke?
Katika mstari huu tunaambiwa ni
nini mtume Paulo alihubiri wakati aliwatembelea watu katika manyumba zao. Aliwaambia, “Inapaswa kumgeukia Mungu kwa
kutubu dhambi na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo.”
1. Inapaswa kumgeukia Mungu kwa kutubu.
Jambo la kwanza kila mtu
anahitaji kufanya akitaka kuokoka ni kutubu dhambi zake. Je, kutubu kunamaanisha nini? Kutubu kunamaanisha mambo mawili.
Kwanza, kutubu kunamaanisha kukubali
kwamba wewe ni mwenye dhambi na kwamba wewe mwenyewe huna uwezo wa
kujiokoa. Unahitaji kufahamu kwamba wewe
huna chochote kizuri ndani yako na wewe huna uwezo hata kidogo wa kumpendeza
Mungu kwa matendo yako. Hata kama
unajaribu sana kumpendeza Mungu kwa matendo yako, hutafaulu. Unahitaji kufahamu kwamba wewe ni mtenda
dhambi. Hili ni jambo ambalo wewe
unahitaji kukubali wakati unakuja mbele za Mungu kwa maombi. Usijaribu kumwambia kwamba wewe ni mtu mwema,
bali kubali mbele zake kwamba wewe uko
na moyo wa dhambi na wewe uko na hatia ya dhambi mbele zake.
Pili, kutubu kunamaanisha
kugeuka kutoka kwa dhambi na kuendelea kugeuka.
Haitoshi kukubali tu kwamba wewe ni mwenye dhambi. Kukubali peke yake haitakuokoa. Unahitaji kuamua kwamba utageuka kutoka kwa
dhambi zako. Unahitaji kuamua kwamba
utaacha milele dhambi zako zote.
Unahitaji kufanya hii maisha yako yote.
Mungu anaamuru kwamba kila mmoja ambaye anakuja kwake kuomba wokovu
ataamua kuacha dhambi zake. Mungu ni
Mtakatifu na mwenye haki na msafi kabisa.
Yeye hatapokea wale ambao wanapenda dhambi zao na hawataki kuziacha. Yeye atawapokea wale tu ambao wameamua
kutoroka dhambi zao.
2. Unahitaji kumwamini Yesu Kristo pekee akuokoe
kutoka kwa dhambi zako.
Ukitaka kuokoka, unahitaji
kugeuka kutoka kwa dhambi zako, na kumgeukia Kristo. Unahitaji kuja kwake Kristo kwa imani na
kumtumainia Yeye pekee kwa wokovu wako. Unahitaji
kwenda kwake kwa maombi na kukubali kwamba wewe huwezi kujiokoa. Unahitaji kumwomba akuokoe. Unahitaji kumwomba aondoe deni la dhambi zako
na kukuosha katika damu Yake. Unahitaji
kumwomba akuondoe kutoka kwa nguvu za dhambi na aondoe ghadhabu ya Mungu ambayo
iko juu yako.
Biblia inatuambia, “Kristo Yesu
alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi” (1 Timotheo 1:15). Hili ndilo lilikuwa lengo lake la kuja hapa
ulimwenguni. Aliishi maisha kamili ili
sisi tuweze kuwa wenye haki kupitia kwa imani ndani yake. Yeye alikufa juu ya msalaba kulipa deni la
dhambi zetu. Alimwaga damu Yake ili sisi
tuweze kuoshwa na kukombolewa kutoka kwa utumwa wa dhambi. Alikufa juu ya msalaba kuondoa ghadhabu ya
Mungu ambayo ilikuwa juu yetu. Yeye
aliteswa ili sisi tuweze kusamehewa, Yeye alikufa ili sisi tuweze kuwa na uzima. Yeye pekee ndiye njia ya kupata msamaha na
kuoshwa na kuokoka. Yeye pekee alitumwa
na Mungu hapa ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi. Yeye pekee alikufa kwa ajili ya wenye dhambi.
3. Ni lazima utubu
na kumwamini Kristo leo.
Umeona kwamba ukitaka kuokoka
unahitaji kugeuka kutoka kwa dhambi zako na kumgeukia Kristo. Ni lazima ufahamu kwamba unahitaji kufanya
hii leo. Usisema, “Siku moja kweli
nitaokoka.”
Unahitaji kuja kwake Kristo leo
kuokoka kwa sababu hujui kama utapata nafasi ya kuja kwake Kristo siku nyingine. Kumbuka kwamba kila siku moyo wako unaendelea
kuwa mgumu kwa sababu ya dhambi zako.
Kila siku moyo wako unapenda dhambi zaidi na zaidi. Ukiacha jambo hili la kuokoka pengine siku
moja hutaweza kutubu na kuamini kwa sababu moyo wako umekuwa mgumu sana.
Kumbuka pia kwamba wewe hujui
ni siku gani utakufa. Pengine leo wewe
ni kijana na uko na afya. Lakini hii
haimaanishi utaishi hapa miaka mingi.
Wengi wanakufa wakiwa vijana.
Jambo hili ni la muhimu sana, usiliache.
Njoo kwake Kristo leo na utaokoka.