Header

Yesu alisema, “Mimi ndimi lango, ye yote anayeingia zizini kwa kupitia Kwangu ataokoka” (Yohana 10:9).

Je, njia ya kufika mbinguni ni gani? Je, ni namna gani mtu anaweza kuhakikisha kwamba wakati atakapokufa, ataingia mbinguni? Maswali haya ni ya muhimu sana kwetu kuwaza juu yake. Sisi sote tunajua kwamba hatutaishi hapa duniani milele, bali siku moja tutakufa. Pia sisi sote tunajua kwamba baada ya maisha hapa ulimwenguni wengine wataenda mbinguni na wengine jahanum. Pia sisi sote tunajua kwamba jahanum ni mahali pa hukumu na adhibu na kuteswa, hapa ni mahali ambapo hakuna yeyte amabye anataka kwenda. Kwa hivyo, je, ni namna gani tunaweza kuhakikisha kwamba tutaingia mbinguni ile siku tutakufa? Majibu ya maswali haya yanapatikana katika maneno haya ya Yesu Kristo.

1. Yesu Kristo ndiye lango la kuingia mbinguni.

Yesu alisema, “Mimi ndimi lango, ye yote anayeingia zizini kupitia Kwangu ataokoka.” Hii inamaanisha kwamba Kristo pekee ndiye njia ya kuingia mbinguni, hakuna njia ingine. Yeye pekee ndiye lango la kuingia mbinguni. Yeyote ambaye anataka wokovu kutoka kwa dhambi zake na kuingia mbinguni anahitaji kuja kwake Kristo. Yeyote akikataa kuja kwake Kristo, basi yeye hataokoka, bali atakuwa jahanum milele.

Tunajua kwamba Kristo pekee ndiye njia ya kuingia mbinguni kwa sababu ni Yeye pekee ambaye alitumwa na Mungu Baba kuwaokoa wenye dhambi. Kabla ya Yeye kuzaliwa malaika alimwambia Yosefu, “Utamwita jina lake Yesu, kwa maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao” (Mathayo 1:21). Huu ulikuwa ujumbe kutoka kwa Mungu kwa Yosefu kumwambia kwamba Kristo alitumwa na Mungu Baba kwa lengo moja: kufungua njia ya mbinguni kwa wale wote ambao watatubu na kumwamini.

Pia, tunajua kwamba Kristo pekee ndiye njia ya kufika mbinguni kwa sababu Yeye pekee alikufa kwa ajili ya wenye dhambi. Biblia inatuambia, “Kristo naye aliteswa mara moja tu, mwenye haki kwa ajili ya wasio na haki, ili awalete ninyi kwa Mungu” (1 Petro 3:18). Hakuna yeyote mwingine ambaye alikufa kwa ajili ya wenye dhambi. Hakuna yeyote mwingine ambaye alidai alikuja hapa ulimwenguni kufa badala ya wenye dhambi. Lakini Yesu alifundisha wazi kwamba lengo lake la kuja hapa ulimwenguni lilikuwa kufa kwa wenye dhambi (Mathayo 16:21).

Pia, tunajua kwamba Kristo pekee ndiye njia ya kufika mbinguni kwa sababu ni Yeye pekee ambaye Mungu Baba alifufua kutoka kwa wafu na kumpatia mwili mpya. Wengine ambao walifanywa hai kama Lazaro hawakupewa miili mipya, lakini wakati Kristo alifufuliwa, alipewa mwili mpya wa milele. Hii inatuonyesha kwamba Mungu Baba alipokea dhabihu yake kwa ajili ya wenye dhambi wakati yeye alikufa msalabani. Yeye pekee aliweza kutoa sadaka kwa ajili ya dhambi zetu kwa sababu yeye pekee aliishi masiha bila dhambi zozote hapa ulimwenguni, na Mungu Baba alipokea sadaka Yake kwa ajili yetu wakati Yeye alimfufua kutoka kwa wafu.

Hii inamaanisha kwamba hakuna njia ingine yoyote kuokoka isipokuwa Kristo. Ukijaribu kujiokoa kupitia kwa matendo yako mema na kazi yako ya dini hutafaulu kamwe. Hii si njia ya kuokoka. Hakuna njia ingine ya kuokoka. Mungu hawezi kubali yeyote aingie mbinguni ambaye anawaza kwamba anaweza kuingia kwa kujaribu kwake; Mungu atawapokea wale tu ambao watakuja kupitia kwa imani ndani ya Kristo.

2. Yesu Kristo anawapokea wote ambao wanakuja kwake.

Yesu Kristo alisema, “Mimi ndimi lango, ye yote anayeingia zizini kwa kupitia Kwangu ataokoka” (Yohana 10:9). Hii inamaanisha kwamba kuna hakikisho hapa. Yeyote ambaye atakuja kwake bila shaka ataokoka. Kifunguo cha mbinguni kiko mikononi Mwake na ni Yeye ambaye anaahidi kwamba wale ambao watakuja kwake bila shaka wataokoka. Yaani, kuna njia ya hakikia ya kuokoka na njia hii ni Yesu Kristo.

3. Ni nini unahitaji kufanya ukitaka kuokoka.

Yesu Kristo alisema, “Wakati umewadia, Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema” (Marko 1:15). Hapa tunaambiwa kwamba kuna mambo mawili tunahitaji kufanya tukitaka kuokoka. Kwanza tunahitaji kutubu. Hii inamaanisha kuziacha dhambi zetu zote. Mtu akiendelea kufuata njia ya dhambi, basi yeye hawezi kuokoka. Unahitaji kuanza kuacha dhambi zako na kuenelea kuziacha maisha yako yote. Mungu ni msafi na mtakatifu na hatakupokea hadi uamue kuziacha dhambi zako.

Pili, unahitaji kumwamini Kristo pekee kwa wokovu wako.

Usiamini matendo yako mema na dini yako kukuokoa. Unahitaji kumwamini Kristo pekee. Yesu Kristo ndiye njia ya kuokoka. Usikae ndani ya dhambi zako. Njoo kwake leo na Yeye atakupokea na kukuokoa.